RATIBA ya Uchaguzi Mkuu Tanzania 2025

RATIBA ya Uchaguzi Mkuu Tanzania 2025
RATIBA ya Uchaguzi Mkuu Tanzania 2025
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jacobs Mwambegele, ameweka wazi ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 wa Rais, Wabunge katika Jamhuri ya Muungano na Madiwani kwa Tanzania Bara.
Akizungumza leo Julai 26, 2025 katika viunga vya Makao Makuu ya Tume hiyo jijini Dodoma, Jaji Mwambegele amesema kuwa Agosti 9 hadi Agosti 27, 2025 itakuwa ni kipindi cha kutoa fomu za uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais.
Jaji Mwambegele amesema kuwa tarehe 09 Agosti, 2025 hadi tarehe 27 Agosti, 2025 itakuwa utoaji wa fomu za uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais.
Tarehe 14 Agosti, 2025 hadi tarehe 27 Agosti, 2025 itakuwa utoaji wa fomu za uteuzi wa wagombea ubunge na udiwani na tarehe 27 Agosti, 2025 itakuwa siku ya uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais, uteuzi wa wagombea ubunge na uteuzi wa wagombea udiwani.
Jaji Mwambegele amesema pia kuwa tarehe 28 Agosti, 2025 hadi tarehe 28 Oktoba, 2025 kitakuwa kipindi cha kampeni za uchaguzi kwa Tanzania Bara na tarehe 28 Agosti, 2025 hadi 27 Oktoba, 2025 kitakuwa kipindi cha Kampeni za Uchaguzi kwa Tanzania Zanzibar Kura.
Jumatano tarehe 29 Oktoba, 2025 ndiyo siku ya Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani kwa Tanzania Bara.
Akazingumza kuhusu idadi ya wapiga kura waliojiandikisha kupiga kura kwenye uchaguzi huo, Jaji Mwambegele amesema jumla ya wapiga kura 37,655,559 wamejiandikisha na kuongeza kuwa idadi hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 26.55 kutoka idadi ya wapiga kura 29,754,699 waliokuwa kwenye daftari, mwaka 2020.
Ameongeza kuwa kwa upande wa Zanzibar, Wapiga Kura 725,876 wapo katika Daftari la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na wapiga kura 278,751 wameandikishwa na INEC kwa kuwa hawakuwa na sifa za kuandikishwa na ZEC.
Katika idadi ya wapiga kura 37,655,559 waliopo katika daftari, wapiga kura 36,650,932 wapo Tanzania Bara na wapiga kura 1,004,627 wapo Tanzania Zanzibar.
Pia ameongeza kuwa kati ya wapiga kura hao, 18,943,455 ni wanawake sawa na asilimia 50.31 na wapiga kura 18,712,104 ni wanaume sawa na asilimia 49.69 na wapiga kura 49,174 ni watu wenye ulemavu.
Aidha jumla ya vituo 99,911 vitatumika kupigia Kura.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia ni Katibu wa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Ramadhani Kailima, amekabidhi Jeshi la Polisi orodha ya watu 8,703 waliokiuka taratibu za kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa kujisajili zaidi ya mara moja.
