VIWANGO Vipya Vya Mishahara ya Sekta Binafsi

VIWANGO Vipya Vya Mishahara ya Sekta Binafsi
VIWANGO Vipya Vya Mishahara ya Sekta Binafsi
Sheria ya Taasisi za Kazi, Sura 300 pamoja na mambo mengine, imempa mamlaka Waziri mwenye dhamana na masuala ya kazi kuunda Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara kwaajili ya kufanya utafiti na kushauri kuhusu viwango vya chini vya mshahara pamoja na masharti mengine ya kazi.
Itakumbukwa kuwa mnamo tarehe 25 Novemba, 2022 aliyekuwa Waziri mwenye dhamana na kazi wa wakati huo alitangaza Kima cha Chini cha Mshahara kwa sekta Binafsi kupitia Gazeti la Serikali, yenye Namba 687.
Aidha, kwa mujibu wa Sheria tajwa Amri hiyo itamaliza muda wake ifikapo Disemba, 2025.
Hivo mchakato wa upangaji wa Kima kipya cha chini cha mshahara umekamilika na kwa kuzingatia mamlaka chini ya Kifungu cha 39 (1) cha Sheria tajwa, Waziri mwenye dhamana ametangaza Amri ya Kima cha Chini cha Mshahara kupitia Gazeti la Serikali la tarehe 13 Oktoba, 2025 yanye Namba 605A.
Kwa mujibu wa Amri hiyo, Sekta za Kima cha chini cha Mshahara zimeongezeka kutoka 13 za mwaka 2022 hadi 16 kwa mwaka 2025 na kutoka sekta ndogo 25 za mwaka 2022 hadi 46 kwa mwaka 2025.
Aidha, Kima cha chini cha mshahara kimeongezeka kwa wastani wa asilimia 33.4 kutoka Shilingi 275,060/= hadi 358,322/=.
Amri ya Kima cha Chini cha Mshahara imegusa sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, afya, mawasiliano, usafirishaji, hoteli, madini, biashara na viwanda, shule binafsi, huduma za ulinzi binafsi, nishati, uvuvi na huduma ya baharini, michezo na utamaduni pamoja na huduma nyinginezo.
Aidha, kwa mujibu wa Amri hiyo, kima cha chini cha mshahara kwa Sekta Binafsi kitaanza kutumika rasmi tarehe 1 January, 2026.
Kima cha chini cha mshahara kimepangwa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali vilivyoainishwa katika Mikataba ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) pamoja na viwango vya kitaifa vilivyoainishwa kupitia Sheria ya Taasisi za Kazi, Sura 300.
Baadhi ya vigezo hivyo ni pamoja na uwezo wa Waajiri kulipa, kupanda kwa gharama za maisha, uwezo wa Waajiri katika kuendesha biashara zao kwa tija pamoja na Dira ya maendeleo ya nchi katika kukuza uchumi, ajira na kazi zenye staha.
Waziri ametoa rai kwa Waajiri wote wa Sekta Binafsi kuzingatia na kutekeleza kima hiki kipya cha mshahara kwa kuwa ni takwa la kisheria.
Ofisi ya Waziri haitasita kuchukua hatua kwa Waajiri watakaokaidi au kushindwa kutekeleza Amri hii kwa makusudi.
Aidha, Ofisi hiyo itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa Amri hii, kutoa elimu kwa Waajiri na Wafanyakazi pamoja na kufanya tathmini ya mara kwa mara ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kikamilifu.
JE, UNATAFUTA AJIRA LEO?Jiunge na Watanzania Wengine Kupata Matangazo ya Ajira Kila Siku Kutoka Serikalini Pamoja na Makampuni Mbalimbali Leo Gusa HAPA
Share Kwa Ndugu, Jamaa na Marafiki nao wapate Fursa hizi Kila Siku.
